OIC yasema, Israel 'inabeba dhima kamili' ya mauaji ya Kiongozi wa HAMAS Ismail Haniya
OIC yasema, Israel 'inabeba dhima kamili' ya mauaji ya Kiongozi wa HAMAS Ismail Haniya
Aug 08, 2024 06:32 UTC
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeulaumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa shambulizi la kigaidi lililomuua Ismail Haniya Mkuu wa Tawi la Kisiasa la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS wiki iliyopita nchini Iran, ambayo Tehran imeapa kuyalipizia kisasi.
Mbali na kulaani mauaji hayo, taarifa iliyotolewa jana
Jumatano baada ya kikao cha dharura cha jumuiya hiyo yenye wanachama 57
kilichofanyika nchini Saudi Arabia imesema "inaibebesha Israel, utawala
unaokalia ardhi kwa mabavu, dhima kamili ya shambulio hilo ovu sana",
ambalo imelitaja kuwa ni "ukiukaji mkubwa" wa mamlaka ya kujitawala ya
Iran.
Kikao cha dharura cha OIC mjini Jeddah kimeitishwa kwa wito uliotolewa na Iran na Palestina.
Katika kikao hicho cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Jumuiya ya
Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Hissein Brahim
Taha, mbali na kulaani mauaji ya Ismail Haniya na ukiukaji wa mamlaka
ya kujitawala ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanywa na utawala wa
Kizayuni katika amesema, jinai hiyo ovu iliyofanywa na utawala wa
Kizayuni ni mwendelezo wa jinai za kivita na mauaji ya kimbari
yanayofanywa kila leo na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya
Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, Ukingo wa Magharibi na Baitul
Muqaddas.
Katika taarifa ya mwisho wa kikao hicho OIC imetahadharisha pia
kuhusu upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za
Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kuendeleza mshikamano
wake imara na taifa la Palestina.
Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na mmoja wa
walinzi wake waliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi iliyotokea mjini
Tehran alfajiri ya kuamkia Jumatano, tarehe 31 Julai.../
Comments
Post a Comment