Uingereza katika dimbwi la ghasia za siasa kali za wafuasi wa mrengo wa kulia
Uingereza katika dimbwi la ghasia za siasa kali za wafuasi wa mrengo wa kulia
Serikali ya Uingereza imeitisha kikao cha dharura ikiwa ni radiamali ya kuenea ghasia na vitendo vya utumiaji mabavu vya wafuasi wa mrengo wa kulia dhidi ya wahamiaji na Waislamu.
Keir Starmer Waziri Mkuu wa Uingereza amelaani shambulizi dhidi ya hoteli moja ya wakimbizi huko Rotherham na kusema kuwa atashughulikia machafuko hayo "kwa kiwango cha juu kabisa cha sheria". Waziri Mkuu wa Uingereza ametaja machafuko hayo kuwa ni vitendo vya "makundi ya kihuni ya watu wa mrengo wa kulia" na kusema "watajuta” kwa vitendo vyao hivyo.
Vitendo vya Uasi na ghasia za makundi ya kibaguzi na yanayopinga wahajiri na Waislamu vimeongezeka katika wiki ya karibuni katika miji kadhaa ya Uingereza. Mashambulizi dhidi ya misikiti, maeneo ya ibada ya Waislamu, makazi ya raia, vituo vya biashara, wizi katika maduka yao na pia mapigano na polisi hadi sasa vimesababisha kujeruhiwa makumi ya watu wakiwemo polisi. Hali hii ya mambo imetajwa kuwa changamoto kwa serikali mpya ya Uingereza. Ghasia zilizoripotiwa katika miji kama vile Liverpool, Leeds na Belfast ziligeuka kuwa machafuko makubwa mwishoni mwa juma, wakati watu wenye siasa kali wa mrengo wa kulia walipopigana na polisi wa kutuliza ghasia, huku kukiripotiwa matukio mengi ya mashambulizi dhidi ya jamii za waliowachache hususan Waislamu katika mitaa ya miji kadhaa ya nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imesema kuwa, "radiamali ya haraka" ya vikosi vya usalama itatumika kuzuia mashambulizi dhidi ya misikiti. Vurugu za ubaguzi wa rangi nchini Uingereza ni moja ya vitendo vya ukatili zaidi vya vikundi vya mrengo wa kulia dhidi ya wahamiaji Waislamu.
Chuki dhidi ya wahamiaji zimeenea nchini Uingereza na katika nchi nyingi za Ulaya. Makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Uingereza na katika nchi nyingi za Ulaya hayaweki waziwazi misimamo yao ya chuki dhidi ya Uislamu. Makundi hayo yanataka kufukuzwa wahamiaji na wakati huo huo yanapinga alama na nembo yoyote ile ya Uislamu, na maeneo ya Kiislamu yanalengwa na kuandamwa na makundi ya mrengo wa kulia na ya ubaguzi wa rangi. Matukio tunayoyashuhudia katika masiku haya katika baadhi ya miji ya Uingereza dhidi ya Waislamu na maeneo ya Kiislamu ni matokeo ya miongo kadhaa ya kuenea chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza na nchi nyingi za bara Ulaya.
Uenezaji wa chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) imekuwa sera ya kimkakati ya serikali ya Uingereza. Serikali ya zamani ya kihafidhina ya Uingereza ilikuwa ikiwaajiri watu wanaopinga Uislamu katika serikali hiyo katika kipindi cha miaka 14 utawala wake na ilikuwa chimbuko la kuibuka na kuenea chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Serikali ya zamani ya kihafidhina ya Uingereza ilikusudia kuzuia shughuli za kijamii za Waislamu wa Uingereza vaada ya kupasisha sheria zenye kuwabana wahamiaji lengo likiwa ni kubinya harakati za kijamii za Waislamu katika nchi hiyo.
Swali linaloulizwa sasa na weledi wa mambo ni je, serikali ya sasa ya Chama cha Leba inayoongozwa na Waziri Mkuu Keir Starmer imekusudia kufuata mkondo wa siasa za kueneza chuki dhidi ya Uislamu zilizokokuwa zikipigiwa upatu na kutekelezwa na serikali iliyopita ya kifadhinian? Bila shaka hilo litafahamika kupitia jinsi serikali ya Uingereza itakavyokabiliana na vitendo vya utumiaji mabavu na vya kibaguzi vya makundi yenye kufurutu ada ya mrengo wa kulia.
Comments
Post a Comment