EU: Hati za kukamatwa za ICC dhidi ya Netanyahu, Gallant na Deif lazima zitekelezwe
EU: Hati za kukamatwa za ICC dhidi ya Netanyahu, Gallant na Deif lazima zitekelezwe
Mkuu wa diplomasia ya Ulaya, Josep Borrell, amebainisha kwamba hati za kukamatwa zilizotolewa Alhamisi na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Waziri wake wa zamani wa Ulinzi, Yoav Gallant, na mwanajeshi mkuu wa Hamas, Mohammed Deif, zinapaswa "kutumika".
Imechapishwa: Imehaririwa:
"Huu sio uamuzi wa kisiasa. Ni uamuzi wa mahakama, mahakama ya haki, mahakama ya kimataifa ya haki. Na uamuzi wa mahakama lazima uheshimiwe na kutumika,” Bw. Borrell amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Amman na mwenzake wa Jordan, Aymane Safadi.
ICC imetoa hati za kukamatwa Alhamisi dhidi ya Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant "kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa angalau kuanzia Oktoba 8, 2023 hadi Mei 20, 2024."
Pia imetoa hati ya kukamatwa kwa Mohammed Deif, mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas ya Palestina "kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa katika nchini Israeli na Palestina tangu angalau Oktoba 7, 2023," tarehe ya shambulio lisilokuwa na kifani la Hamas dhidi ya Israel kutoka Gaza ambalo lilizua vita vya sasa.
Uamuzi wa ICC kinadharia unaweka ukomo wa safari za Benjamin Netanyahu, kwani nchi yoyote kati ya 124 wanachama wa mahakama hiyo italazimika kumkamata katika ardhi yake.
"Uamuzi huu ni wa lazima, na Mataifa yote, nchi zote zinazohusika na sheria ya mahakama, ikiwa ni pamoja na wanachama wote wa Umoja wa Ulaya, wanatakiwa kutekeleza uamuzi huu wa mahakama," Bw. Borrell amesema.
Kulingana na Israel, Mohammed Deif aliuawa katika shambulio la Julai 13 kusini mwa Gaza, lakini Hamas inakanusha kifo chake.
Bw Borrell, waziri wa zamani wa Uhispania, anatazamiwa kuondoka madarakani mwezi ujao na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Estonia, Kaja Kallas.
Comments
Post a Comment