Mabadiliko ya Katiba nchini DRC: Wapinzani waahidi maandamano

 

Mabadiliko ya Katiba nchini DRC: Wapinzani waahidi maandamano

Viongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameahidi maandamano siku ya Jumatano kupinga mapendekezo ya mabadiliko ya katiba yaliyotangazwa na Rais Tshisekedi, anayetuhumiwa kutaka "kusalia madarakani milele".

Upinzani wa Kongo unamtuhumu Bw. Tshisekedi kwa kutaka "kugombea muhula wa tatu" kwa kuongoza kile wanachoeleza kuwa "mapinduzi ya kikatiba".
Upinzani wa Kongo unamtuhumu Bw. Tshisekedi kwa kutaka "kugombea muhula wa tatu" kwa kuongoza kile wanachoeleza kuwa "mapinduzi ya kikatiba". © AP
Matangazo ya kibiashara

Félix Tshisekedi, 61, alichaguliwa tena mwezi Desemba kwa muhula wa pili. Katiba inasema kuwa nchini DRC rais anaweza kuchaguliwa kwa "mamlaka ya miaka mitano ambayo inaweza kurejelewa upya mara moja tu".

"Watu wa Kongo, huu ni wakati mzito, tuamke," amehimiza Devos Kitoko, katibu mkuu wa Ecidé, chama cha mpinzani na mgombea katika uchaguzi uliopita wa rais Martin Fayulu, wakati wa mkutano wa waandishi wa habari pamoja na vyama kadhaa vya upinzani.

Wawakilishi wa chama cha rais wa zamani Joseph.Kabila na chama cha mfanyabiashara tajiri Moïse Katumbi, pia mgombea urais, walikuwepo.

Katika taarifa ya pamoja, wapinzani wamemshutumu Bw. Tshisekedi kwa kutaka "kugombea muhula wa tatu" kwa kuongoza kile wanachoeleza kuwa "mapinduzi ya kikatiba" na kulaani "utawala wa kiimla".

"Maandamano ya raia kote nchini na walioko ughaibuni yatafanyika katika siku zijazo ili kutetea Katiba yetu na kuzuia njia ya Bw. Félix Tshisekedi," wameahidi.

Katika wiki za hivi karibuni, Félix Tshisekedi mara kadhaa alithibitisha nia yake thabiti ya kutekeleza marekebisho ya Katiba, bila hata hivyo kubainisha kama hii itakuwa ni marekebisho ya baadhi ya Ibara au kupitishwa kwa nakal mpya.

Mwaka 2015, maandamano yalizuka hasa katika mji mkuu wa Kinshasa na Goma (mashariki), kupinga sheria ya uchaguzi ambayo ingeweza kumuwezesha Joseph.Kabila kusalia madarakani zaidi ya mihula miwili. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu kadhaa na hatimaye Kabila hakushiriki uchaguzi wa urais wa mwaka 2018.

Nchini DRC, marekebisho yoyote ya Katiba lazima yaidhinishwe "kwa kura ya maoni kwa wito wa Rais wa Jamhuri" isipokuwa mradi huo uidhinishwe na wingi wa 3/5 wa Bunge.

Katiba ya Kongo ilitangazwa mwaka 2006 na Kabila. Ilirekebishwa mnamo mwaka 2011, haswa kuleta upigaji kura kwa wote kwa duru moja badala ya mbili hapo awali.

Comments

Popular posts from this blog

Mali: Wanachama wa Azimio la Machi 31 watoa wito wa kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa

Raia wa Somaliland, eneo lililojitenga na Somalia wanashiriki uchaguzi mkuu

Iran yailaani Daesh (ISIS) kwa kumuua waziri wa serikali Taliban Afghanistan